Nov 19, 2010

CHADEMA WAGOMEA MATOKEO.

Chadema: Hatutambui matokeo ya urais 2010, MTIKILA AMSHANGAA SLAA KUKAA KIMYA Send to a friend
Tuesday, 16 November 2010 05:56
0diggsdigg
Waandishi Wetu, Dodoma na Dar
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), kimetangaza kuwa hakitambui matokeo ya uchaguzi wa urais wa Jamhuri ya Muungano yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi (Nec), na kwamba hakimtambui Rais Jakaya Kikwete kama rais wa Tanzania.

Tamko hilo la kwanza la aina yake tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi, lilitolewa jana mjini Dodoma na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, katika siku ambayo mwenyekiti wa DP, Mch Christopher Mtikila alidai kuwa mgombea wa urais wa Chadema, Dk Willibrod Slaa aliibuka na ushindi wa asilimia 71 na kushangaa katibu huyo mkuu wa Chadema kutochukua hatua.

Mbowe aliwaambioa waandishi wa habari jana kuwa uamuzi wao unatokana na kasoro kubwa zilizojitokeza katika ujumlishaji wa kura na utangazaji matokeo, ambazo alisema zililenga kumpa ushindi mgombea wa CCM na hivyo kukubali matokeo itakuwa ni sawa na kuhalalisha matokeo ya kura haramu.

"Katika mazingira haya ya kikatiba na kisheria, njia pekee tuliyonayo ya kuonyesha kutoridhika kwetu na ukiukwaji huu wa makusudi wa nguzo kuu za uchaguzi huru na wa haki, ni kuheshimu dhamiri zetu kwa kutoyatambua matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi," inasema taarifa ya Chadema iliyosomwa mbele ya waandishi na mwenyekiti huyo ambaye pia ni mbunge wa Hai.

Akiwa pamoja na Dk Slaa na viongozi wengine wa chama hicho, Mbowe alisema wanajua kuwa uamuzi wao hauwezi kubadilisha matokeo wala kumzuia aliyetangazwa kuwa rais kufanya kazi zake.

"Hata hivyo, hatuko tayari kuhalalisha matokeo yaliyotokana na ukiukwaji wa makusudi wa katiba, sheria za uchaguzi na kanuni zinazotambuliwa kimataifa za uchaguzi huru na wa haki," alisema Mbowe.

"Kufanya hivyo itakuwa ni sawa na kuwaambia wananchi wa Tanzania kwamba kupiga kwao kura hakuna maana yoyote kama tutakuwa tunakubali kuhalalisha matokeo ya kura haramu.

“Uamuzi wetu wa kutokuyatambua matokeo ya uchaguzi wa rais, haumaanishi kwamba wawakilishi wa Chadema bungeni na katika halmashauri mbalimbali za wilaya na za miji wataacha kazi zao.

Wabunge na madiwani wetu wataendeleza utumishi wa umma ndani ya vyombo husika vya maamuzi kwa kutanguliza mbele maslahi ya taifa.”

Mbowe alifafanua maslahi hayo ya taifa kuwa ni "kama kupambana na ufisadi, kusimamia rasilimali za nchi na kutetea sera mbadala zenye kutoa fursa kwa wananchi walio wengi kwenye sekta za kiuchumi, kijamii na kisiasa".

Mbowe, ambaye chama chake kimeunda kambi ya upinzani bungeni anayoiongoza baada ya kukidhi kanuni za bunge kwa kuwa na wabunge 45, alisema wabunge wake watakuwepo ndani ya ukumbi wa Bunge wakati Rais Jakaya Kikwete atakapohutubia Novemba 18 licha ya uamuzi huo wa kutomtambua.

Kiongozi huyo wa upinzani bungeni alisema Chadema itatoa maelezo kadiri muda unavyokwenda kuhusu uamuzi wao kuhudhuria uzinduzi wa Bunge.

Alisema nje ya Bunge na vyombo vingine vya maamuzi, chama kitasimamia ajenda husika ikiwemo kuunganisha watanzania katika kudai katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.

Kutokana na madai hayo ya ukiukwaji wa taratibu uliofanya uchaguzi usiwe huru na wa haki, Chadema inataka kuundwa kwa tume huru itakayochunguza mchakato mzima wa uchaguzi pamoja na sababu za msingi zilizofanya idadi kubwa ya wananchi waliojiandikisha katika daftari la wapigakura kutokupiga kura.

Akielezea jinsi chama hicho kilivyofikia uamuzi wa kutomtambua mshindi wa kiti cha urais, Mbowe alisema kabla ya kutangazwa rasmi kwa matokeo ya rais, Chadema iliitaka Nec kusitisha kutangaza matokeo kutokana na kuwepo kwa kasoro nyingi katika zoezi zima la ujumlishaji na utangazaji matokeo.

Mbowe alisema kasoro kubwa ilikuwa ni kitendo cha Nec kubadilisha matokeo ya kura kutoka majimbo ya uchaguzi kwa lengo la kumwongezea mgombea wa CCM kura na hivyo kumpa ushindi mkubwa kuliko waliyompa wapigakura wa Tanzania.

“Kasoro za namna hiyo hiyo zimejitokeza katika majimbo na kata mbalimbali kwa upande wa nafasi ya ubunge na udiwani,” alisema Mbowe ambaye chama chake kililalamikia matokeo ya uchaguzi wa urais katika majimbo ya Geita, Hai na Segerea na baadaye Nec ikabaini kuwa kulikuwa na makosa ya utangazaji wa matokeo ya urais kwenye Jimbo la Geita.

Aliongeza kuwa ni katika mazingira hayo waliiomba Nec kusitisha zoezi hilo lakini kama ilivyofahamika tume iliendelea na zoezi hilo na baadaye kumtangaza mgombea wa CCM kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi wa rais.

“Pamoja na uchakachuaji huu wa makusudi matokeo ya uchaguzi kwa lengo la kunufaisha CCM, sisi tumekuwa na uvumilivu mkubwa tukiongozwa na dhamira yetu ya kulinda amani ya nchi yetu. Tunatambua kwamba kwa utaratibu uliopo sasa hivi kikatiba na kisheria, uchakachuaji huu wa matokeo ya uchaguzi wa rais hauwezi kupingwa katika mahakama au chombo chochote kilichoundwa kikatiba,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema wanatambua kwamba kwa katiba na sheria za sasa, Nec inalindwa kisheria hata kama inachakachua matokeo ya uchaguzi kwa makusudi kwa lengo la kunufaisha chama tawala.

Alisema kuwa tamko la kina kuhusu mapungufu yaliyojitokeza, mafanikio yaliyopatikana na mwelekeo wa chama katika kipindi cha miaka mitano ijayo litatolewa baada ya ripoti ya tathimini kuwasilishwa kwenye kamati kuu na baraza kuu la Chadema na kwamba mipango mbalimbali inaandaliwa.

Akijibu hoja iliyotaka kujua Chadema itapokea vipi iwapo wabunge wake watateuliwa na rais kuwemo katika Baraza la Mawaziri, Mbowe alisema kuwa "hilo likitokea tutafanya kazi pamoja na kuwa hatumtambui rais... lakini Chadema haipo kwa ajili ya vyeo bali kwa maslahi ya Watanzania".

Awali aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Dk Willibrod Slaa alisema kuwa tangu awali aliyakataa matokeo ya rais aliyechaguliwa na hamtambui Kikwete akisistiza kuwa uamuzi huo ni wake mwenyewe usiokuwa na msukumo wa mtu.

“Hatukuwa na uchaguzi huru na wa haki hivyo, sijayumba katika tamko hili. Tuliwaeleza Nec kuhusu hili, lakini hatua hazijachukuliwa na hawajatujibu chochote,” alisema Dk Slaa.

Alisema kutokana na hilo amekabidhi rasmi majukumu kwa chama ili kiweze kuchukua hatua na mwenyekiti ndiye mwenye jukumu hilo.

Wakati Chadema ikitoa tamko lake mjini Dodoma, Mch Mtikila aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuwaeleza kuwa Dk Slaa ndiye aliyeibuka mshindi wa uchaguzi wa rais huku akimshangaa kwa kukaa kimya wakati aliibiwa kura.

Mtikila, aliyezungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam, alidai kuwa kwa mujibu wa vyanzo vyake na watu alionao karibu, Dk Slaa alipata asilimia 70 ya kura zilizopigwa.

Mwanasiasa huyo alidai kuwa kura alizopata Rais Jakaya Kikwete aliyetangazwa mshindi hazikuzidi milioni mbili na kwamba matokeo ya uchaguzi huo yalichakachuliwa.

“Dk Slaa alikuwa mshindi lakini matokeo yalichakachuliwa... naona yuko kimya, sasa sijui karidhika au vipi,” alisema Mchungaji Mtikila.

"Waangalizi wa kimataifa walikuwa mashahidi katika uchaguzi wa mwaka huu, Nec wenyewe walichakachua majina ya waliopiga kura na idadi ya waliojiandikisha; wao wanachojua ni kulinda kura za CCM tu.”

Alisema kuwa umefikia wakati wa kufutwa kwa kipengere cha sheria kinachokataza matokeo ya urais kupingwa mahakamani na kwamba sheria hiyo ikiendelea kuwepo inaweza kuwafanya Watanzania kushika mitutu kwa kuwa kadri miaka inavyozidi kwenda ndivyo matokeo ya uchaguzi yanavyozidi kujaa dhuruma.
Hatua hiyo ya Chadema imepokelewa kwa hisia tofauti na wasomi na wanasiasa na wanasheria, baadhi wakionyesha kushangazwa na hatua hiyo, wengi wakisema haitakuwa na madhara makubwa.

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Felix Kibodya alisema ameshangazwa na tamko hilo la Chadema na kuhoji Mbowe atafanyaje kazi kama kiongozi wa upinzani bungeni katika masuala ya kutunga sheria huku akiwa hamtambui rais aliyepo madarakani ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kusaini au kupitisha sheria hizo.

“Kisheria na kikatiba Bunge ni wabunge na rais. Bila ya rais hamna bunge kwa sababu wabunge ni watunga sheria rais anaidhinisha matumizi ya sheria hiyo. Sasa kama hamtambui rais atafanyaje kazi,” alihoji Kibodya.

“Rais akishatangazwa na kuapishwa, kikatiba na kisheria msimamo wa chama ni kitu kingine na kumtambua au kutomtambua ni kingine. Lakini msimamo huo hauna athari yeyote kwa rais,” aliongeza Kibodya.
Profesa Abdallah Safar alisema katika uhusiano wa kimataifa kuna aina mbili za serikali ambazo ni serikali iliyo madarakani kwa mujibu wa sheria (de jure) na serikali iliyo madarakani kwa nguvu (de facto).

Alifafanua kuwa ni bora kuwapo kwa hiyo serikali isiyokubalika ili kuepuka matatizo mbalimbali ambayo yangetokana na ukosefu wa uongozi kwa sababu “ni bora nusu shari kuliko shari kamili.”

“Lakini ili kuepuka ‘vacuum’ (ombwe) la uongozi lazima iwepo hata kama haikubaliki. Na sharti ni kwamba lazima kufanyike uchaguzi katika muda uliopangwa kikatiba, hii ni kama serikali ya mpito,” alisema Profesa Safar.

Lakini profesa Safar alihoji kuwa, “Je Mbowe hatambui mahakama, polisi, magereza na taasisi nyingine za serikali?.”

Alisema kitendo cha Chadema kumkataa rais kinaweza kuwakosesha mambo mengi ambayo wangetakiwa kuyapata na hawatakuwa na mtu wa kumlaumu.

“Waswahili wanasema 'wakiranga haliliwi wala hawekewi matanga’ na 'msiba wa kujitakia hauna pole',” alisema Profesa Safari.

“Japokuwa serikali yetu ni ‘defacto’ lakini kama mtu amefanya mambo ambayo baadaye yanamsababishia matatizo, hana wa kumlaumu wala wa kumlilia kwa sababu amefanya kusudi.”

Mhadhiri wa kitivo cha Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Bashiru Ally alisema pamoja na mambo mengine tamko la Chadema halina madhara makubwa kutokana na sheria kutoruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani,.

“Hapo ndipo unapoonekana umuhimu wa kuwepo kwa sheria itakayoruhusu matokeo ya uchaguzi wa rais kupigwa mahakamani,’’ alisema Ally

Ally, ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya siasa za ndani na kimataifa, alisema hata kama Chadema wana ushahidi wa kutosha kuhusu hali halisi ya uchaguzi ulivyokuwa, hakuna chombo kitakachoweza kuthibitisha hilo.

Hata hivyo, aliishauri Chadema kutoa hadharani ushahidi walionao kuhusu uchakachuaji uliofanyika katika uchaguzi mkuu ili wananchi waelewe.

Katika hatua nyinyine, Mchungaji Christopher Mtikila wa DP amesema atafungua kesi mahakamani kupinga uamuzi wa Nec kumuengua katika kinyang’anyiro cha urais.

Mtikila, ambaye alienguliwa kwa madai ya kutotimiza masharti ya kuwa na wadhamini 200 katika mikoa 10 ya Tanzania Bara, alisema kuwa Watanzania zaidi ya milioni 10 ambao hawakupiga kura katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31 mwaka huu, walifanya hivyo kwa kuwa hakugombea urais.

“Ndio; waliojiandisha kupiga kura walikuwa watu karibu milioni 20, lakini waliojitokeza kupiga kura walikuwa milioni 8.4, kati ya hao waliomchagua aliyekuwa mgombea wa CCM walikuwa milioni 5.8. Sasa hawa ambao hawakujitokeza kupiga kura wangenichagua mimi kwa sababu ya itikadi na sera zangu za kuleta ukombozi nchini Tanzania,” alisema Mtikila.

Mtikila alisema kutokana na hali hiyo ameiandika Nec barua akiitaka kufanya upya uchaguzi wa urais kwa kuwa haikumtendea haki.

Imeandaliwa na Boniface Meena, Dodoma na Fidelis Butahe,Sadick Mtulya na Salim Said, Dar es Salaam